Ijumaa , 16th Nov , 2018

Aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage ameibuka na kuzungumza bungeni, kwa mara ya kwanza tangu atenguliwe nafasi yake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli wiki iliyopita.

Aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage.

Akizungumza Bungeni Jijini Dodoma kabla hajauliza swali kwa Wizara ya Nishati, Mwijage amelishukuru bunge hilo kupitia kwa Spika Job Ndugai wakati wote wa Uwaziri wake ndani ya Bunge, akisema,

Nawashukru sana tangu mlivyokuwa mkiniongoza bungeni, kupitia kwako Mwenyekiti napenda kumshukuru Rais,  Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kwa namna ambavyo waliniamini na kunisimamia kwenye majukumu ambayo waliyonipa.”

Wiki iliyopita, Rais Magufuli alipokuwa akiwaapisha mawaziri wapya wawili na naibu mawaziri wanne, alibainisha kuwa Charles Mwijage, na Charles Tizeba walishindwa kufanya maamuzi wakati wafanyabiashara wa korosho waliposhindwa kununua korosho za wakulima.

"Nilimwambia Waziri Mkuu awakumbushe mawaziri wake, kwa sababu matatizo mengi yaliyokuwa yakihusu kilimo na viwanda yalikua yanamalizwa na Waziri Mkuu, nilijiuliza pia kahawa ni kilimo pia vipi Waziri hakuliona pia." Rais Magufuli.

"Nilijiuliza kwanini hawa tuliowapa ,majukumu hawafanyi hivi, ni ukweli pia bei ya soko la korosho limeshuka kidogo unapoona kuna tatizo unamtuma Waziri Mkuu anatatua," aliongeza Rais Magufuli.