Alhamisi , 5th Jan , 2023

Jalada la kesi namba 11 ya mwaka 2022 ya usafirishaji haramu wa binadamu, inayomkabili  Mfalme Zumaridi, limefikishwa mikononi mwa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa serikali (DPP) Sylvester Mwakitalu, kufuatia upelelezi wake kutokamilika tangu Februari, 2022, Zumaridi alipokamatwa.

Mfalme Zumaridi (kulia), akiwa mahakamani

Wakili wa Mfalme Zumaridi, Erick Mutta, alihoji upande wa mashtaka kutokamilisha upelelezi wa kesi hiyo huku mteja wake Zumaridi akiendelea kusota rumande katika gereza kuu la Butimba ndipo Mwendesha Mashtaka wa serikali Mwanahawa Changale, akadai kuwa jalada la kesi hiyo tayari lipo mikononi mwa DPP Sylvester Mwakitalu

Aidha Mwendesha Mashtaka huyo wa serikali Mwanahawa Changale, ameieleza mahakama hiyo kuwa Januari 13 mwaka huu ofisi ya mwendesha mashtaka wa serikali itatoa maamuzi maamuzi ya kesi hiyo

Katika hatua nyingine hukumu ya kesi namba 10 inayomkabili Mfalme Zumaridi na wafuasi wake nane imekwama tena katika Mahakama ya Hakimu mkazi mkoa wa Mwanza baada ya Hakimu Mfawidhi Monica Ndyekobora, kutokuwepo mahakamani kwa madai kuwa yupo likizo.