Kigwangalla akubali yaishe sanamu la Nyerere

Alhamisi , 11th Jul , 2019

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt Hamis Kigwangalla , ameomba kupewa muda ili kurekebesha mfano wa sanamu ambalo lilichongwa kuashiria kuwa ni Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, ambalo hivi karibuni lilizua mjadala mkubwa hususani kwenye mitandao ya kijamii.

Katika uzinduzi wa hifadhi ya Burigi iliyoko Wilaya Chato mkoani Geita Waziri Kigwangala, alimkabidhi Rais Magufuli mfano wa sanamu la Mwalimu Nyerere, huku watu mbalimbali wakidai sanamu hilo halina uhalisia na Mwalimu Nyerere.

Waziri Kigwangalla amesema kuwa "Baba wa Taifa alitoa tamko la kwanza la Uhifadhi nchini, ambalo ndiyo dira yetu, tuache dhihaka kwa sababu hakuna aliyefanya kazi ile kwa kusudi hilo, tumesema linashughulikiwa tunaomba mtuamini, mtupe muda turekebishe."

"Kilichonifurahisha ni kuwa kizazi cha vijana wa kisasa, bado kinamkumbuka vizuri Baba wa Taifa, kinamuenzi na kumheshimu sana, ndiyo maana wanaikumbuka taswira yake, tutatumia vizuri zaidi wataalamu wetu kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza kabla ya kuitumia" ameongeza Kigwangalla

Hivi karibuni kwenye uzinduzi wa hifadhi ya Burigi Waziri Kigwangalla alimkabidhi tuzo maalum ambayo hifadhi ya Taifa ya Serengeti ilishinda kwa ni hifadhi bora barani Afrika.