Jumatano , 12th Aug , 2020

Aliyekuwa Mbunge wa Ubungo kupitia CHADEMA, Saed Kubenea amesema yeye kutokugombea tena jimbo hilo na kwenda Kinondoni si kwamba anamuogopa mgombea wa jimbo hilo kupitia CHADEMA bali ameamua kurudi nyumbani na amefanya hivyo kwa kuwa hataki dhambi ambayo ingesaidia Jimbo hilo kwenda CCM.

Mgombea Ubunge Jimbo la Kinondoni, Saed Kubenea.

Kubenea ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na EATV&EA Radio Digital, na kuongeza kuwa yeye amekuwa maarufu kabla ya Boniface Jacob na hivyo ameamua kumpisha kwa sababu amekuwa akitamani siku nyingi kumuona akiwa ni Mbunge.

"Nawezaje kumkimbia Boniface, mimi nimekuwa mashuhuri kabla yake, mimi napenda awe Mbunge na ashinde, lakini mimi chama changu cha ACT kina mgombea pale na napenda hao watu wawili wakae wakubaliane kwa sababu kuna hatari hilo Jimbo kwenda CCM, nimuogope Boniface kwanini nisiwaogope CCM, kwanini nisimuogope Tarimba, kina Iddi Azan nimuogope yeye na mimi sina tabia ya kuogopa", amesema Kubenea.

Aidha Kubenea amezitaja sababu zilizopelekea kutokugombea jimbo hilo la Ubungo ni kutokana na migogoro iliyokuwepo awali kwenye chama chake cha CHADEMA ikiwemo kusakamwa bila sababu za msingi.