Jumanne , 11th Feb , 2020

Katibu wa Uenezi wa Chama cha ACT Wazalendo, Ado Shaibu amesema kuwa Kiongozi wa Chama hicho Zitto Kabwe, hajashindwa kurejea nyumbani kwa sababu ya hofu na vitisho anavyovipata bali ni kutokana na afya yake kutokuwa imara na Madaktari kumshauri apumzike.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe

Akizungumza leo Februari 11, 2020 na EATV&EA Radio Digital, Ado Shaibu amesema kuwa Zitto alitarajiwa kurudi nchini siku ya jana ila kutokana na hali yake kutokuwa nzuri alishindwa, ila kwa sasa anaendelea vizuri na kwamba tarehe 18 lazima atahudhuria mahakamani ili kujua hatma yake.

"Zitto anaumwa na atarudi nyumbani, si kama kashindwa sababu ya hofu, sisi tunaamini kwamba majaribio yote ya kumdhuru Zitto hayawezi kufanikiwa, alitoa kauli zile za kupokea vitisho kwa sababu ilikuwa ni muhimu kupaza sauti ili kuzuia uovu" amesema Ado Shaibu.

Jana Februari 10, 2020 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam mdhamini wa Zitto Kabwe, Ray Kimbita aliiambia Mahakama kuwa Zitto ameshindwa kuhudhuria mahakamani kwasababu ni mgonjwa na amelazwa Marekani.