Alhamisi , 3rd Nov , 2022

Hospitali ya Kanda ya Rufaa ya Chato, kwa kushirikiana na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, wamezindua kliniki ya wagonjwa wa moyo kwenye hospitali hiyo ili kuwapunguzia adha wananchi wa kanda ya ziwa kusafiri zaidi ya kilomita 100 kufuata huduma ya matibabu hayo jijini Dar es Salaam.

Bia

Akizungumza mara baada ya kuzindua Kliniki hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Dkt. Peter Kisenge, amesema serikali kwa kutambua umuhimu wa huduma ya matibabu ya Moyo imeandaa mkakati ndani ya miaka mitano.

"Tunakwenda kutengeneza mpango mkakati wa kuhakikisha katika miaka mitano huduma hizi za upasuaji wa Moyo na matibabu kwa kutumia mtambo wa Katla unafanyika hapa Chato na huduma hizi zitawasaidia wananchi hapa Chato na mikoa yote ya pembezoni, kama tunavyofahamu hata Hospitali ya Bugando kwa sasa hivi haina Katla, lakini Katla ikiletwa hapa, ukipata mshtuko ghafla wa Moyo, basi utakuja Chato utapata huduma," amesema Dkt. Kisenge.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi wa Taasii hiyo Profesa William Mahalu anaelezea sababu zinazopelekea watu kupata magonjwa ya Moyo.

"Sigara kwa kweli zimefahamika, kuna utafiti wa kutosha kusema zinaleta magonjwa ya Moyo, zinaleta magonjwa ya mishipa ya damu, zinaleta magonjwa ya mishipa ya fahamu unasikia wana ganzi, zimeleta matatizo ya Ubongo, la mwisho ni pombe, pombe sasa hivi utafiti umekuwa ukisuasua na kupishana kwanza walisema pombe ziachwe, nasikia wanasema sasa hivi, kunywa bia yako lakini shida uinywe bia moja kwa muda wa lisaa limoja, unywe polepole ili Ile level ya damu yako isipande kufikia kiasi kile ambacho kinaweza kudhuru Figo na viungo nilivyovitaja", alisema Mahalu.