Jumatatu , 24th Sep , 2018

Mbunge wa Iringa Mjini Mchungaji Peter Msigwa amesema hata akikabidhiwa ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) hawezi kuipokea kwa madai kila mwananchi anapaswa kukabidhiwa mpango wa maendeleo ya taifa ya miaka mitano na si ilani ya CCM.

Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa.

Kauli hiyo imekuja kufuatia www.eatv.tv ilipomtafuta mbunge huyo wa Chadema Jimbo la Iringa mjini baada hivi karibuni kukaririwa kwenye mitandao ya kijamii akiikosoa kitendo cha baadhi ya viongozi wa serikali kutaka kila mtumishi wa umma kuwa na ilani ya chama hicho tawala.

Mchungaji Msigwa amesema "ilani inafanywa kuwa Mpango wa miaka mitano na ukishapitishwa unatungiwa sheria, hatutekelezi ilani ya Chama cha Mapinduzi, kwa hiyo mtu akisema tunatekeleza ilani ya CCM anapoteza muda tu, kwa sababu hakuna nguvu ya kisheria ya kutekeleza ilani ya CCM ila kuna nguvu ya kissheria kutekeleza mpango wa miaka 5, kwa hiyo ukinipa ilani ya CCM ni sawa umenipa gazeti tu."

www.eatv.tv imezungumza na Katibu wa Bunge wa Stephen Kagaigai juu ya namna ambavyo ya utekelezaji wa zoezi la uongezwaji kwa ilani ya CCM kwenye makablasha ya wabunge amesema yeye bado hajakadhiwa ilani kwa ajili ya kuwakabidhi.

"Hizo ilani sizigawi mimi, ni serikalini huko, kwenye makablasha yangu sikuziona na kama walipewa labda walipewa kwa njia nyingine ila kwenye makashablasha yangu sijaziona." Amesema Katibu wa bunge Kagaigai

Katika bunge la mwezi April mwaka huu Spika wa bunge Job Ndugai alitoa mwongozo kwa katibu wa bunge juu ya ugawaji wa ilani ya CCM kwa wabunge wa upinzani.