Jumanne , 16th Oct , 2018

Waziri Kivuli wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Godbless Lema ametumia dakika 44 kujibu lililokuwa hitaji la Mbunge wa Kigoma mjini, Zitto Kabwe juu ya kutoa tamko kuhusu tukio la kupotea kwa mfanyabiashara maarufu
nchini Mohamed Dewji.

Godbless Lema

Hivi karibuni Zitto alikuwa akimshinikiza Mbunge huyo wa Arusha mjini kuzungumza juu ya taarifa ya matukio ya kupotea kwa watu siku chache kufuatia kupotea kwa Mo Dewji ikiwa ni baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Kangi Lugola kusema kuwa katika kwa kipindi cha Miaka 3 zaidi ya watu 75 walitajwa kupotea.

Katika mkutano na wanahabari leo jijini Dar es salaam, Godbless Lema amesema kuwa tukio la kupotea kwa mfanyabiashara huyo linaathiri taswira ya Tanzania hasa kwenye masuala ya uwekezaji.

Watu wengi duniani wameona tukio la kidnaped (utekaji), leo hii habari zinaenda kwa matajiri duniani, hawa ndio wanahamasisha uwekezaji, mmeona kwenye vyombo vikubwa vya habari duniani. Matokeo yake kwenye uchumi ni kubwa mno, kama tungekuwa kwenye stock market(soko la hisa) mngeona shilingi inashuka. Watu wenye mitaji wataondoa mitaji yao kwa ajili ya kukwepa usalama wataenda kwenye nchi jirani”, amesema Lema.

Kupitia mtandao wa Twitter, Zitto Kabwe aliandika "ndugu @godbless_lema kwenye utamaduni wa Jumuiya ya Madola, Waziri mwenye dhamana akitoa kauli, lazima Waziri Kivuli wa sekta hiyo atoe kauli pia ama kuunga mkono au kupingana na ya Waziri mwenye dhamana, tunasubiri kauli yako. Nchi inasubiri. Kukaa kimya nikukubaliana na Kangi."

Alhamis ya wiki iliyopita kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii nchini kulianza kusambaa taarifa juu ya kupotea kwa Mfanyabiashara maarufu nchini Mohamed Dewji ambaye inasemekana amechukuliwa na watu wasiojulikana.

Jeshi la Polisi hii leo limewaachia kwa dhamana watu 19 kati ya 26 ambao walikamatwa kwa mahojiano, akiwemo Afisa Habari wa klabu ya Simba, Haji Manara ikiwa ni sehemu ya upelelezi wa tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara huyo. Familia ya Mohammed Dewji imetangaza kutoa donge nono la shilingi bilioni 1 kwa atakayesaidia kutoa taarifa za ukweli za kupatikana kwake.