
Kamanda wa Polisi Mkoani Mwanza, Jonathan Shana
Kamanda Shana ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na www.eatv.tv baada ya kusambaa kwa taarifa kuwa Jeshi la polisi limelazimika kutumia nguvu ya ziada kuwazuia wafanyabiashara wa soko la Mlango Mmoja jijini humo.
“Hizo taarifa za kuwa kuna vurugu si kweli hakuna mgomo wowote, ungekuwepo mgomo ungesikia tumewasha moto. Walikuwa na kikao chao cha kujadili mambo yao wamejadili kwa amani na wametawanyika kwa amani,” amesema Kamanda Shana.
“Na kama wanadai kuna picha zinaonesha askari wetu wanatumia nguvu kuwaondoa wafanyabiashara hao niletee mimi nakupa milioni 10 sasa hivi,” ameongeza Kamanda Shana.
Awali ilielezwa kuwa wafanyabiashara katika soko la Mlango Mmoja jijini Mwanza wamefanya mgomo ndani ya soko hilo kwa kile walichokidai kuwa Halmashauri ya jiji hilo imeshindwa kuwapatia vibali vya ujenzi wa maduka yao 29 pamoja na vibanda 55 vilivyoteketea kwa moto.