Lindi : Aliyembaka mtoto wa miaka 10 ahukumiwa

Ijumaa , 23rd Aug , 2019

Mahakama ya Wilaya ya Lindi imemuhukumu bwana Issa Seif Mpanyanje (51) kifungo cha miaka (30) gerezani, baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mtoto wa miaka kumi.

Hukumu hiyo imetolewa na Mahakama hiyo, chini ya Hakimu Liliani Rualabamo, baada ya kuridhishwa bila shaka, na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka.

Hakimu Rugalabamo akitoa adhabu katika kesi hiyo, amesema kutokana na sheria kumshika mikono, amemuhukumu kwenda gerezani miaka 30 na atakapomaliza adhabu yake amlipe mlalamikaji fidia ya Sh. milioni 2.

Awali ilidaiwa Mahakama ilielezwa kuwa mshtakiwa kwa kutambua anachokifanya ni kosa, April 14, 2019, maeneo ya mashambani, alimbaka mlalamikaji na kumsababishia maumivu makali sehemu zake za siri.

Aidha mshtakiwa alimshawishi mlalamikaji waende Shambani akamsaidie kuvuna karanga na baada ya kufika huko shamba alianza kumtomasa tomasa, kisha kumbaka huku akimtaka kutomwambia mtu yeyote.