Ijumaa , 18th Dec , 2015

Mwanasheria mkuu wa zamani wa Tanzania, Jaji Mark Bomani, anasema hali ya kisiasa visiwani Zanzibar inatishia mustakabali wa eneo hilo na kama uchaguzi mpya utafanyika basi lazima usimamiwe na jopo maalumu la wataalamu.

Jaji Mark Boman akiongea na waandishi wa habari

Katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, mwanasheria huyo amesema kuwa kile kinachoendelea visiwani humo hakiashirii picha njema hivyo akashauri kuchukuliwa kwa hatua za kibusara kwa ajili ya kukwamua mzozo huo.

Ikiwa ni kauli yake ya kwanza tangu kufutwa kwa uchaguzi huo miezi miwili iliyopita, Jaji Bomani amesema kuwa iwapo hali hiyo itaachwa iendelee inaweza kusababisha madhara makubwa jambo ambalo linaweza kuirudisha nyuma Zanzibar.

Kauli hiyo imekuja huku kukiwa na ripoti kwamba viongozi wa pande zote CCM na CUF wamekuwa wakikutana mara kwa mara Ikulu ya Zanzibar katika kile kinachoelezwa kuwa ni jitihada za kujaribu kutanzua hali hiyo.

Tangu kuanza kwa vikao hivyo hakuna upande uliokuwa tayari kuelezea maendeleo yaliyofikiwa huku baadhi ya maofisa wa CUF wakiendelea kusisitiza haja ya kutolewa kwa matokeo ya uchaguzi huo ambao ulifutwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi wa Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha.

Ama mwanasheria huyo ambaye amekuwa akitokeza mara kwa mara kutoa maoni yake pindi kunapojitokeza utata katika masuala ya kitaifa, amesema kuwa pande zote mbili yaani CCM na CUF bado haziaminiani hivyo iwapo hata kutarudiwa kwa uchaguzi huo hali itajirudia ile ile.

Kwa maana hiyo alitaka kuundwa kwa jopo maalumu la wataalamu wa mambo ikiwamo kutoka jumuiya ya kimataifa ili kushughulikia uchaguzi mwingine.