Jumatano , 17th Dec , 2025

Hukumu hiyo imetolewa juzi Desemba 15, 2025, na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Augustine Rwizile, baada ya ushahidi uliowasilishwa mahakamani kubaini kuwa mauaji hayo yalitekelezwa na maafisa hao.

Maafisa watatu wa Uhamiaji, Fredrick Kyomo, Joachim Trathizius na Mabruki Hatibu, wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa na Mahakama Kuu ya Tanzania baada ya kupatikana na hatia ya kumuua Enos Elias, mkazi wa Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma, aliyekuwa akishukiwa kuwa si raia wa Tanzania.

Hukumu hiyo imetolewa juzi Desemba 15, 2025, na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Augustine Rwizile, baada ya ushahidi uliowasilishwa mahakamani kubaini kuwa mauaji hayo yalitekelezwa na maafisa hao.

Katika hukumu yake, Jaji Rwizile alieleza kuwa upande wa mashtaka uliwasilisha ushahidi wa kutosha uliothibitisha kuwa watuhumiwa walihusika moja kwa moja katika tukio la mauaji, na kwamba hakuna mtu mwingine au kundi jingine lililohusika katika kifo cha marehemu.

Mahakama ilisisitiza kuwa vitendo vilivyofanywa na maafisa hao ni kinyume cha sheria, maadili ya utumishi wa umma na haki za binadamu, na kwamba hukumu hiyo ni funzo kwa watumishi wa umma kuzingatia sheria na taratibu wanapotekeleza majukumu yao.

Kwa uamuzi huo, Mahakama Kuu imewaamuru watuhumiwa hao wanyongwe hadi kufa kwa mujibu wa sheria za nchi.