Jumanne , 17th Sep , 2019

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, ametengua uteuzi wa Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mkoani Morogoro Majura Mateko Kasika, na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi Mussa Elias Mnyeti.

Barua iliyotumwa kupitia Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu Gerson Msigwa, imesema utenguzi wa wa Mkuu huyo wa Wilaya ya na Mkurugenzi umeanza leo, na nafasi zao zitajazwa baadaye.

Taarifa hiyo imesema kuwa "Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mkoani Morogoro Majura Mateko Kasika na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi Bw. Mussa Elias Mnyeti".

"Uteuzi wa viongozi hao umetenguliwa kuanzia leo Septemba 17, 2019, na uteuzi wa viongozi watakaojaza nafasi hizo utafanyika baadaye." imesema taarifa hiyo.

Jana Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alipofanya ziara wilayani humo alibainisha kuchukizwa na mgongano uliopo kati ya Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Majura Kasika na Mkurugenzi Mussa Mnyeti, na kumuagiza Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, kuchunguza utendaji kazi wao.