Jumatatu , 5th Oct , 2015

Mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli Kesho ataunguruma katika mkoa wa Arusha, kwenye viwanja vya mpira Sheikh Amir Abeid, akitokea wilayani karatu, ambako pia leo atafanya mkutano wa hadhara wa kampeni.

Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli

Akizungumzia ziara hiyo katibu wa CCM, mkoa wa Arusha Alphonce Kinamhala, amesema Dk. Mgufuli alipokelewa katika Kijiji cha Kansay wilayani karatu jana, akitokea wilayani Mbulu mkoa wa Manyara, alikwenda moja kwa moja, kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni mjini Karatu.

Kinamhala, amesema kesho asubuhi Dk. Magufuli ataelekea wilayani Monduli ambapo atafanya mkutano wa hadhara wa kampeni eneo la Mto wa Mbu na mara baada ya mkutano huo atafanya mkutano mwingine mkubwa wa hadhara, kwenye ngome ya Lowassa Mjini Monduli, kisha kuelekea wilayani Longido kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni.

Amesema mara baada ya mkutano huo ataelekea jijini Arusha, kwa ajili ya mkutano mwingine wa hadhara wa kampeni utakaofanyika katika viwanja wa Sheikh Amir Abeid majira ya saa 8:00 mchana na mara baada ya mkutano huo ataelekea wilayani Arumeru ambapo atafanya mkutano wa hadhara katika viwanja vya Ngarasero eneo la Usa River.

Baada ya hapo Dk. Magufuli ataondoka kuelekea Sanya Juu, mkoani Kilimanjaro kwenye mkutano wa hadahara.