
Rais Magufuli akimpongeza Anna Mghwira baada ya kumuapisha kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.
Rais Magufuli amefunguka sababu hizo wakati wa hafla ya kumuapisha Mghwira iliyofanyika leo Ikulu Dar es Salaam na kuhurudhuriwa viongozi mbalimbali na kumwambia aende kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa ili kuondoa kero zinazowakabili wananchi wa mkoa huo bila ya kujali itikadi za vyama vya siasa, dini, makabila na kanda wanazotoka.
“Mimi huwa siteui watu hivi hivi, huwa naangalia uwezo wa mtu, na wewe nimekuchunguza na nimejiridhisha kuwa una uwezo wa kuwatumikia wananchi, nenda kachape kazi, kawaondolee kero wananchi wa Kilimanjaro, wapo watu watakaokusema na wengine watakuonea wivu, kutoka hata ndani ya chama chako au CHADEMA na hata CCM wewe kachape kazi usiwasikilize” alisema Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli amemhakikishia Bi. Mghwira kuwa atapata ushirikiano wa kutosha wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yake na asikubali kuyumbushwa na mtu yeyote katika majukumu yake ya kuwa hudumia wananchi.
Kwa upande wake Bi. Mghwira amemshukuru Rais Magufuli kwa kumuamini na kumteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro huku akimuahidi kuwa yupo tayari kwenda kufanya kazi ya kuwatumikia wananchi na kujenga taifa.
“Ninasema hii ni heshima kwa taifa letu, ni heshima kwa umoja wa nchi yetu, ni heshima kwa siasa za umoja wa nchi yetu, kumekuwa na minong’ono mingi sana kuwa Rais analeta nini, kuteua watu wanaitwa wapinzani, mimi sio mpinzani wa maendeleo” alisema Mghwira.