Jumatatu , 1st Jun , 2020

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo, amesema kuwa ile Tweet yake ya jana ya kwamba alipoteuliwa kwenye nafasi hiyo watu walimbeza na kumkejeli na kusema kuwa hilo halikuiwa dongo kwa mtu yeyote yule, bali alikuwa anajaribu kuelezea safari ya mwanadamu ilivyo fumbo kama kilivyo kifo.

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo.

DC Jokate ameyabainisha hayo leo Juni Mosi, 2020, wakati wa mazungumo maalum kwenye kipindi cha SupaBreakfast ya East Africa Radio, na kusema kuwa maisha ya mwanadamu ni safari na hakuna anayeijua safari ya mwenzake na safari ikishaanza basi ni wachache sana ambao watakuunga mkono.

"Lile halikuwa dongo ilikuwa ni kuelezea safari ya mwanadamu, kwa sababu maisha ni fumbo, kama ilivyokuwa kifo, maisha ni safari na hakuna anayeijua safari ya mwenzake na kila hatua unayoipiga siyo kila mtu atakuunga wala kukutia moyo, unapoona hivyo siyo kwamba ufe moyo wewe songa mbele" amesema DC Jokate.

Jana kupitia ukurasa wake wa Twitter, mara baada ya Shule ya Sekondari ya Kisarawe kupewa jina lake aliandika hivi, "Nilipoteuliwa wapo walibeza na wengine kujaribu kunivua utu wangu, niliwaelewa lakini, Pwani wanasema Aso Mtu Ana Mungu, Namshukuru Mungu wangu kwa kunitetea. Mhe Waziri Jafo kamuelekeza DED kuisajili hii shule ya kihistoria Kisarawe na iitwe Jokate Mwegelo Girls Secondary School".