Jumanne , 5th Jan , 2016

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekagua maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kanda ya Songea, wakati akiendelea na ziara yake mkoani Ruvuma.

Waziri Mkuu, Kassim Majliwa akikagua mahindi yaliyohifadhiwa nje ya majengo ya maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula NFRA mjini Songea

Akizungumza na wafanyakazi wa Wakala hiyo, wadau wa kilimo pamoja na wananchi jana, (Jumatatu, Januari 4, 2016) nje ya majengo ya Wakala mara baada ya kukagua mahindi yaliyohifadhiwa katika maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kanda ya Songea , mkoani Ruvuma amesema kufuatia taarifa ya kuwepo na baadhi ya maeneo yenye njaa nchini, Serikali imetoa tamko kuwa hakuna mtanzania atayakekufa kwa njaa.

Ambapo, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kitengo cha Maafa imeweka mikakati ya kukabiliana na tatizo la njaa kwa kutoa msaada wa chakula katika maeneo yanayokabiliwa na njaa.

“Ni wajibu wangu kuhakikisha nasimamia vizuri hili, nimeona hali ya uhifadhi wa chakula, tunayo mahindi ya kutosha lakini hakuna sehemu ya kuhifadhi chakula” amesema Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu Majaliwa ameendelea kwa kusema uwezo wa maghala hayo yaliyopo chini ya Wakala Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kanda ya Songea yana uwezo wa kuhifadhi tani 29 pekee na Songea inauwezo wa kuzalisha zaidi tani 70 hadi 80.

Pia , ameagiza Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kanda ya Songea , kuanzia mwaka huu kwa kushirikiana na Wakuu wa Mikoa pamoja Wakuu wa Wilaya kuanzisha vituo vya kununulia mahindi na kuhakikisha magunia yanawafikia wakulima katika vituo hivyo ambapo wataweza kuhifadhi mahindi na kuuza kwa bei ya kwenye soko.

Waziri Mkuu pia, ameitaka Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kanda ya Songea ,kutumia teknolojia ya kisasa ya uhifadhi wa chakula, kuandaa utaratibu maalum utakaozuia msongamano wa malori yanayosubiri kupata huduma ya kununua mahindi nje ya majengo ya Wakala na kukamilisha miradi itakayosaidia Wakala kuwa na fedha za kutekeleza majukumu yake.

Kwa upande wake, Meneja Hifadhi wa Chakula kanda ya Songea, Bwana. Morgan Mwaipaya amesema kati ya maghala 33 ya kuhifadhi mahindi nchi nzima, Songea ina maghala 6 kati ya hayo. Hivyo, Wakala imeweka vipaumbele vyake ambavyo ni pamoja na kutoa chakula cha msaada kwa maeneo yenye matatizo ya njaa, kuongeza upatikanaji wa mahindi ili kuzuia kupanda kwa bei ya chakula mwaka 2015 – 2016, Wakala kununua na kuhifadhi mahindi katika maeneo yaliyozalisha zaidi na kuzingatia sehemu ya sehemu ya akiba ya chakula na kuuza kwa wakulima, mawakala pamoja na Wakala wa Chakula duniani (World food program).

Amesema Wakala imeandaa mikakati ya mbalimbali ikiwemo kuongeza uwezo wa tani 24600 hadi tani 45000 kwa mwaka 2014- 2017, kuboresha mfumo wa utendaji kazi kwa kutumia mifumo ya stahili ya TEHAMA na kutumia fursa za mikopo kutoka Taasisi mbalimbali za kifedha ili kuendesha shughuli za uwezeshaji I kiwemo kuelimisha taratibu za ununuzi kwa mawakala.

Naye, Mbunge wa Jimbo la Songea, Mhe.Leonidas Gama amesema wakulima wachache wamekua wakiuza mahindi yao kwa bei ya soko, wengi wao wamekua wakiuza mahindi kwa mawakala kwa bei ya shilingi 150 hadi 200 kwa kilo na wakala wakiuza kwa shilingi 500 kwa Serikali. Ambapo amemuomba Waziri Mkuu kutatua tatizo la soko la mahindi kwa wakulima. Hata hivyo Waziri Mkuu ametoa wito kwa wakulima kuendelea kuzalisha mahindi akiahidi Serikali kununua mahindi hayo kwa bei ya soko ambayo itamnufaisha mkulima.

Waziri Mkuu Majaliwa anaendelea na ziara mkoani Ruvuma, leo siku ya jumanne(Januari 5, 2016) atatembelea na kukagua Hospitali ya Rufaa ya Mkoa na kuongea na Watumishi wa hospitali hiyo na baadae ataongea na Watumishi wa Umma.