Jumamosi , 18th Jun , 2022

Waziri mkuu Kassim Majaliwa amezitaka taasisi zote zenye dhamana ya masuala ya ardhi na makazi kuhakikisha zinakuja na mikakati thabiti ya kutatua migogoro ya matumizi ya ardhi iliyoainishwa wakati wa utekelezaji wa zoezi la operesheni ya anuani na makazi.

Waziri Mkuu ametoa wito huo leo Juni 18, 2022 wakati akipokea taarifa ya utekelezaji wa zoezi la operesheni ya anuani na makazi, kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu amewataka viongozi katika ngazi zote hususan kwenye Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za mitaa kuhakikisha wanasimamia kikamilifu utunzaji wa mifumo sambamba na kulinda miundombinu ya anwani za makazi kwenye maeneo yao.

“Pia toeni miongozo ya namna bora ya kushughulikia changamoto za Watanzania wenzetu kuishi katika maeneo yasiyoruhusiwa kisheria Ili kuhakikisha wananchi wote wananufaika na fursa zitokanazo na zoezi hili” Amesema Kassim Majaliwa Waziri Mkuu

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amesema kuwa hadi kufikia Mei 31, 2022 kupitia operesheni ya anuani na makazi  taarifa na anuani za makazi 12,385,956 zilikusanywa sawa asilimia 106.94 ya lengo lililokusudiwa.

“hii ni zaidi ya lengo tulilojiwekea awali la kukusanya taarifa na kutoa anuani za makazi 11,582,106” amesema Waziri wa habari Nape Nnauye