Jumapili , 11th Feb , 2024

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuongoza mazishi ya Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa, yanayotarajiwa kufanyika wilayani Monduli mkoani Arusha Jumamosi Februari 17, 2024.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimpa pole Mjane wa aliyekua Waziri Mkuu Mstaafu, Marehemu Edward Lowassa, Regina Lowassa, nyumbani kwake Masaki, jijini Dar es Salaam, Februari 11.2024.

Waziri Mkuu ameyasema hayo jana Jumapilii, Februari 11, 2024, wakati akitoa taarifa ya ratiba ya mazishi ya kiongozi huyo, Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu Oysterbay, Dar es Salaam.

Amesema katika kipindi cha siku tano za maombolezo, Taifa litaendelea na shughuli za umma na kijamii sambamba na kushirikiana na wanafamilia katika ratiba ya msiba kama ilivyoandaliwa na kamati ya mazishi ya Kitaifa na wanafamilia.

Amesema kabla ya mazishi hayo mwili wa Hayati Lowassa unatarajiwa kuagwa katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam na Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Amesema Jumanne Februari 13, 2024 mwili wa Hayati Lowasa unatarajiwa kuangwa na viongozi na wananchi katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu amesema Jumatano Februari 14 mwili wa Hayari Lowasa  utapelekwa katika Kanisa la KKKT Azania Front kwa ajili ya ibada takatifu na kuaga na kwamba Alhamisi Februari 15 mwili wa Hayati Lowassa utasafirishwa hadi jijini Arusha ambapo viongozi na wananchi watapa fursa ya kuaga katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid.

Waziri Mkuu huyo mstaafu alifariki jana (Jumamosi, Februari 10, 2024) wakati akipatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam na tangazo la kifo chake lilitolewa na Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango.