Alhamisi , 31st Oct , 2019

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda, amepokea hundi ya malipo yenye thamani Shilingi Milioni 27, fedha ambazo zitatumika kuwakatia bima ya afya watoto 500, waliofanyiwa na watakaofanyiwa upasuaji wa moyo, kutoka katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.

RC Makonda akiwa na Balozi kutoka nchi za Falme za Kiarabu

Akizungumza leo Oktoba 31, 2019, wakati akipokea hundi hiyo ya malipo kutoka kwa Balozi wa nchi za Falme za Kiarabu, Makonda amemshukuru Balozi huyo kwa kuwa mstari wa mbele, kuhakikisha anarudisha tabasamu kwa familia ambazo hazikuwa na uwezo wa kugharamia matibabu ya watoto wao.

"Watoto wote walioko Muhimbili wanaofanyiwa upasuaji, sasa ninaenda kuwalipia bima ya afya ya mwaka mzima, Wazazi wao hawatahangaika tena kulipa gharama yoyote ya matibabu, wapo ambao tayari washafanyiwa upasuaji na majina yao tunayo lakini, mwishoni mwa Mwaka tutafanya kampeni ya kuchangia matibabu ya watoto 500 na wao wataingia kwenye huu mfumo wa kupatiwa bima za afya" amesema Makonda.

Kampeni hii ya kuchangia matibabu kwa watoto wenye matatizo ya moyo, wanaotoka katika familia zenye kipato cha chini, ilianzishwa na Mkuu huyo wa Mkoa na alisema atahakikisha kila mwezi, zinapatikana fedha za kufanyiwa upasuaji watoto 10.