Jumapili , 17th Sep , 2023

Mataifa matatu ya Afrika Magharibi ya Sahel yanayotawaliwa na wanajeshi Mali, Niger na Burkina Faso yametia saini mkataba wa usalama siku ya Jumamosi na kuahidi kusaidiana iwapo kutatokea uasi wowote au uvamizi kutoka nje.

Nchi hizo tatu zinajitahidi kuwadhibiti waasi wa Kiislamu wanaohusishwa na al Qaeda na Islamic State na pia zimeshuhudia uhusiano wao na majirani na washirika wa kimataifa ukidorora kwa sababu ya mapinduzi hayo.

Mapinduzi ya hivi punde nchini Niger yalizua mvutano zaidi kati ya nchi hizo tatu na nchi za jumuiya ya kikanda, Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi, ambayo imetishia kutumia nguvu kurejesha utawala wa kikatiba nchini humo.

"Shambulio lolote dhidi ya mamlaka na uadilifu wa eneo la pande moja au zaidi zilizo na kandarasi litachukuliwa kuwa uchokozi dhidi ya pande zingine kulingana na hati ya makubaliano inayojulikana kama Muungano wa Nchi za Sahel "-Kiongozi wa junta wa Mali Assimi Goita amesema kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X (Twitter).

Mataifa yote matatu yalikuwa wanachama wa kikosi cha pamoja cha G5 Sahel kinachoungwa mkono na Ufaransa na Chad na Mauritania kilichoanzishwa mwaka 2017 ili kukabiliana na makundi ya yenye itikadi kali katika eneo hilo.

Mali imeachana na shirika hilo baada ya mapinduzi ya kijeshi wakati Rais wa Niger aliyeondolewa madarakani Mohamed Bazoum alisema mwezi Mei mwaka jana kwamba shirika hilo sasa limekufa kufuatia kuondoka kwa Mali.

Uhusiano kati ya Ufaransa na mataifa hayo matatu umedorora tangu mapinduzi.

Ufaransa imelazimika kuondoa wanajeshi wake kutoka Mali na Burkina Faso na iko katika mvutano mkali na utawala wa kijeshi ulionyakua mamlaka nchini Niger baada ya kuitaka iondoe wanajeshi wake na balozi wake.

Ufaransa imekataa kutambua mamlaka ya junta.