Jumatatu , 1st Mei , 2023

Sehemu za makazi ya kuwahifadhi wahamiaji katika jiji la Texas nchini Marekani zimezidiwa uwezo kutokana na wimbi kubwa la wahamiaji ambao mamlaka imesema wanamiminika kwa wingi.

Maelfu ya wahamiaji kutoka Mexico, wanawapa kazi ngumu maafisa wa Marekani kuhudumia makundi makubwa ya watu wanaokimbia umaskini na vurugu kwenye nchi yao.

Wahamiaji wengi waliofika katika mji wa Brownsville kusini mwa Texas wamepelekea watoa huduma za kijamii kuelemewa na kusababisha kukataliwa baadhi ya wahamiaji katika sehemu za kuwasaidia watu hao. Maafisa wamesema zaidi ya wahamiaji 15,000, wengi wao kutoka Venezuela, wiki iliyopita walivuka mto ulio karibu na mji huo wa Brownsville kinyume cha sheria.

Maafisa wa Forodha na Ulinzi wa Mipaka katika jimbo la Texas wamesema hilo ni ongezeko kubwa la wahamiaji ukilinganisha na watu 1,700 walioingia kwenye eneo hilo wiki mbili za kwanza za mwezi huu wa Aprili.