Ijumaa , 15th Mei , 2015

Jeshi la polisi mkoa wa Manyara limepiga marufuku utengenezaji holela wa milipuko ya kienyeji inayotajwa kushamiri katika migodi ya wachimbaji wadogo wa madini ya Tanzanite Mererani ambayo imekuwa ikisababisha madhara ya vifo kwa wachimbaji.

Kamanda wa Jeshi la polisi Mkoa wa Manyara Christopher Fuime.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara Christopher Fuime ametoa kauli hiyo alipokuwa anazungumza na wachimbaji wadogo katika kikao cha kujadili hali ya usalama sehemu ya machimbo kilicho wahusisha wachimbaji wadogo, maafisa madini na wataalam wa milipiko kutoka jeshi la wananchi (JWTZ).

Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji wadogo wa madini mkoa wa Manyara Sadick Menene amekiri kuwepo kwa baadhi ya wachimbaji wanaotengeneza milipuko ya kienyeji na kuitumia kujeruhi wachimbaji wenzao.

Kutokana na kadhia hiyo baadhi ya viongozi wa wachimbaji hao wametaka vyombo vya sheria kuwachukulia hatua wale wote wanaojihusisha na vitendo hivyo.

Katika kikao hicho, mtalamu wa milipuko kutoka jeshi la wananchi wa Tanzania Fredy Athumani amelazimika kutoa elimu ya utunzaji wa milupuko na madhara ya kutengeneza milipuko ya kienyeji

Utengenezaji holela wa milipuko unatajwa kusababisha madhara na vifo kwa wachimbaji huku baadhi yao wakidaiwa kuitumia kinyume na taratibu kwa kulipuana wenyewe kwa wenyewe na kuhatarisha usalama katika migodi.