Alhamisi , 24th Jul , 2014

Chama cha Madaktari nchini Tanzania kimelaani kitendo cha kutupwa kwa viungo vya binadamu nje ya jiji la Dar es Salaam kinyume cha sheria.

Rais wa chama cha madaktari nchini Tanzania - MAT, Dkt Primus Saidia.

Akizungumza jijini Dar es salaam Rais wa chama hicho, Dk. Primus Saidia ametaka hatua madhubuti zichukuliwe dhidi ya wahusika ikiwemo kupigwa marufuku kwa mtu au taasisi kuendesha shughuli zozote za utafiti kwa kutumia viungo vya binadamu.

Dk Primus ameweka bayana kwamba, licha ya fani hiyo ya udaktari kuruhusiwa kutumia viungo vya binadamu katika shughuli mbali mbali za utafiti kwa mujibu wa sheria za kitaifa na kimataifa lakini ameelezea kwamba kitendo hicho kimekiuka haki za binadamu.

Wakati huo huo, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu LHRC kimezitaka mamlaka zote zinahusika na usajili na usimamizi wa mafunzo ya taaluma za afya nchini kuchukua hatua kali dhidi ya Chuo kikuu cha Teknolojia na Tiba IMTU kutokana na uzembe uliohusika na kusababisha sakata la viungo vya binadamu kuzagaa na kusababisha taharuki kwa watu.

Katika taarifa yake, kituo hicho kimesema kitendo cha viungo vya binadamu kumwagwa hovyo kama ilivyotokea hivi karibuni huko Bunju A nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, ni udhalilishaji mkubwa wa utu wa mwanadamu na kwamba haikustahili kitendo hicho kufanywa na taasisi inayoheshimika kama chuo kikuu.