Jumapili , 18th Aug , 2019

Jumla ya wasichana 170 katika shule ya Sekondari Tura iliyopo Uyui Tabora,  wamepata taulo za kike watakazotumia kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Makabidhiano ya taulo za kike katika Shule ya Sekondari ya Tura

Shule hiyo iliyopo zaidi ya kilometa 150 kutoka Tabora mjini ni shule ya Bweni kwa wasichana ambapo Mkuu wa shule hiyo Adam Shaban Mangao, ameeleza kuwa taulo hizo zitasaidia kupunguza matatizo kwa wanafunzi wawapo bwenini.

''Kampeni ya Namthamini itatatua tatizo wanafunzi kubaki bwenini na kukosa masomo maana ndio tatizo ambalo limekuwa likisababisha kupunguza ufaulu kutokana na watoto hawa kulazimika kukosa vipindi wanapokuwa kwenye hedhi lakini hawajatumiwa fedha za kujikimu na kuweza kununua taulo hizi'', amesema.

Aidha Mwalimu Mangao, amezipongeza na kuzishukuru East Africa Television na East East Africa Radio kwa kuichagua shule ya Tura, kuwa miongoni mwa shule nyingi zitakazofikiwa na Kampeni ya Namthamini mwaka huu.

Zoezi la ugawaji wa taulo za kike katika shule 4 za mkoani Tabora lilikamilika Jumamosi Agosti 17, 2019, ambapo zaidi ya wanafunzi 500 wamepata taulo za kike kwa mwaka mzima.

Shule nyingine zilizofikiwa katika mkoa huo ni pamoja na Ikomwa, Ndono pamoja na Idete, ambapo timu ya East Africa Television na East Africa Radio iliambatana na mkuu wa mkoa huo Aggrey Mwanri.

Katika mwaka wake wa tatu, Namthamini imefanikiwa kufika katika mikoa ya Manyara, Arusha na Tabora huku ikitarajiwa kufika katika mikoa mingine ikiwemo Dodoma.