Alhamisi , 15th Nov , 2018

Mbunge wa Jimbo la Tandahimba, mkoani Mtwara kupitia Chama cha Wananchi CUF, Katani Ahmadi Katani, amekanusha tuhuma zinazogaa mtandaoni kuwa amejiuzulu na kujivua uanachama wa chama chake.

Jengo la Bunge.

Akizungumza na www.eatv.tv Katani amesema kuwa hawezi kufanya hivyo kwani atakuwa amewakosea wapiga kura wake, na hayuko tayari kujiuzulu hadi chama kichoke kimfukuze.

Katani ameongeza kuwa hawezi kujiuzulu ubunge na kisha kugombea tena nafasi hiyo kwani atakuwa hajakitendea haki chama chake kilichompa dhamana.

"Nani kasema nmejiuzulu, najiuzulu ili nifanye nini? nimeziona hizi taarifa kuanzia juzi lakini leo zimesambazwa kwa kasi sana", amesema Katani.

Mapema leo zilisambaa taarifa kuwa Mbunge wa Jimbo la Tandahimba, Mtwara, kupitia Chama cha Wananchi CUF, Katani Ahmadi Katani naye amejiuzulu Ubunge na nafasi zake zote ndani ya CUF, kutokana na chama chake kuwa na migogoro isiyokwisha, inayoathiri utendaji kazi wake.