Jumanne , 8th Dec , 2015

Mfumuko wa bei unaopimwa kwa kigezo cha mwaka nchini Tanzania, umeongezeka kutoka kiwango cha asilimia sita nukta tatu ilivyokuwa mwezi Oktoba

Mfumuko wa bei unaopimwa kwa kigezo cha mwaka nchini Tanzania, umeongezeka kutoka kiwango cha asilimia sita nukta tatu ilivyokuwa mwezi Oktoba, na kufikia asilimia sita nukta sita mwezi Novemba mwaka huu, huku bei kubwa ya bidhaa za vyakula na nishati ikiwa moja ya chanzo cha ongezeko hilo la mfumuko wa bei.

Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Kijamii wa ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Bw. Ephraim Kwesigabo, amesema hayo leo na kwamba katika kipindi hicho, thamani ya shilingi ya Tanzania nayo imezidi kuporomoka ambapo kila shilingi mia moja inaweza kufanya manunuzi ya shilingi sitini na mbili na senti thelathini na moja kutoka shilingi sitini na mbili na senti themanini na mbili.

Bw. Kwesigabo ameongeza kuwa ongezeko la mfumuko wa bei limeshuhudiwa pia katika nchi nyingine za Afrika Mashariki, ambapo nchini Kenya mfumuko umepanda kutoka asilimia 6.72 hadi asilimia 7.32, wakati nchini Uganda mfumuko umepaa kutoka asilimia 8.8 hadi asilimia 9.1.