Jumatano , 18th Jun , 2025

Mhubiri mwenye utata kutoka Kenya Gilbert Deya, aliyedai kuwa na uwezo wa kuwapa wanawake mimba za kimiujiza, amefariki katika ajali ya barabarani.

Polisi Kenya wamesema kuwa Deya alifariki papo hapo Jumanne jioni baada ya gari lake kuhusika katika ajali na basi la chuo kikuu na gari jingine karibu na mji wa Kisumu magharibi mwa Kenya.

Takriban watu wengine 30 waliripotiwa kujeruhiwa, akiwemo mtu aliyetambuliwa kuwa mke wake na abiria kwenye gari lake, na wanafunzi 15 waliokuwa katika basi.

Deya, ambaye alikuwa akiendesha kanisa moja mjini London, alijizolea umaarufu mkubwa mwanzoni mwa miaka ya 2000, kufuatia madai yake kwamba angeweza kuwasaidia wanandoa wenye changamoto za uzazi kupata watoto wa "miujiza" kupitia maombi.

Uchunguzi baadaye ulihusisha kanisa lake na kundi linalodaiwa kuwa la ulanguzi wa watoto, na kusababisha kukamatwa kwake na kurejeshwa nchini kutoka Uingereza takriban miaka minane iliyopita baada ya vita vya kisheria vilivyodumu kwa muongo mmoja.

Aliondolewa mashtaka hayo miaka miwili iliyopita kutokana na kutokuwa na ushahidi wa kutosha. #EastAfricaTV 
Leo, 18/06/2025, Gavana wa Kaunti ya Siaya James Orengo alisema amepokea kwa "huzuni kubwa kifo cha mhubiri Gilbert Deya".

Alithibitisha kuwa ajali hiyo "ya kutisha" ya barabarani ilihusisha gari la kaunti hiyo.