Jumanne , 23rd Nov , 2021

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa zile tozo nzuri zenye lengo la kuendelea kuliletea Taifa maendeleo zitaendelea kuwepo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan

Kauli hiyo ameitoa hii leo Novemba 23, 2021, mkoani Arusha wakati wa maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani, wakati akikataa ombi lililotolewa na Jeshi la Polisi nchini kwamba nusu ya tozo zinazotokana na faini ya makosa barabarani zitumiwe na jeshi hilo.

"Na ninaposema neno tozo, huwa linanigusa ndani ya moyo maana mitandaoni huko wananiita Bi Tozo, lakini Bi Tozo kwa njia nzuri ya maendeleo ya Taifa letu na zitaendelea kuwepo," amesema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia amesema, "Mmekuja na pendekezo kwamba mruhusiwe kutumia nusu ya fedha zinazokusanywa kwenye tozo mbalimbali za makosa ya barabarani, wazo ambalo binafsi siliungi mkono, tozo zile tumeziweka ni adhabu kwa wakosaji, sasa tukiruhusu nguvu nyingi itatumika kwenye kutoza kuliko kudhibiti”.