Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limethibitisha kukamilika kwa maandalizi yote ya Mtihani wa Kidato cha Nne (CSEE) unaotarajiwa kuanza kesho Novemba 17 hadi Desemba 5, 2025, katika vituo 5,868 vya shule na 813 vya watahiniwa wa kujitegemea.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Nov 16,2025 jijini Dar es salaam Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Prof. Said Mohamed, amesema maandalizi yamefanyika kwa umakini ili kuhakikisha mtihani unafanyika kwa amani na uadilifu.
“Kwa mwaka 2025, jumla ya watahiniwa 595,816 wamesajiliwa kufanya mtihani huo, wakiwemo 569,914 wa shule na 25,902 wa kujitegemea. Kati ya watahiniwa wa shule, wasichana ni 303,886 sawa na asilimia 53.32, huku wavulana wakiwa 266,028 sawa na asilimia 46.68. Aidha, watahiniwa 1,128 wa shule na 56 wa kujitegemea ni wenye mahitaji maalum, hatua ambayo imeifanya NECTA kuweka miundombinu maalum ya kuwawezesha kufanya mtihani bila vikwazo”, amsema Prof. Mohamed.
Akizungumzia maandalizi,amesema Baraza limekamilisha maandalizi yote ikiwa ni pamoja na usambazaji wa mitihani, nyaraka na vifaa kwa halmashauri zote Tanzania Bara na Zanzibar.
Vilevile, Kamati za Mitihani za mikoa na halmashauri zimetoa mafunzo kwa wasimamizi na kuhakikisha vituo vina usalama wa kutosha. Maandalizi ya watahiniwa wenye mahitaji maalum yamekamilika ikiwemo maandishi ya nukta nundu, maandishi makubwa na muda wa nyongeza kwa mujibu wa miongozo.
Baraza pia limezitaka Kamati za Mitihani kuhakikisha usalama wa vituo na kuzingatia miongozo iliyotolewa ili kuzuia mianya ya udanganyifu huku likitoa wito Kwa wasimamizi, kufanya kazi kwa uadilifu, kutotengeneza mazingira ya upendeleo na kuhakikisha kila mtahiniwa anapata haki yake bila usumbufu.
Kwa upande wa watahiniwa, Prof. Mohamed amewataka kuzingatia kanuni za mitihani na kuepuka vitendo vya udanganyifu ambavyo vinaweza kusababisha matokeo kufutwa. Ameeleza kuwa walimu wamewajengea msingi mzuri na sasa jukumu liko kwao kufanya kwa bidii na kufuata taratibu zilizowekwa.
