Jumatatu , 25th Jan , 2016

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa Bwana Dickson E. MAIMU, kuanzia leo, tarehe 25 Januari, 2016.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa Bwana Dickson E. MAIMU, kuanzia leo, tarehe 25 Januari, 2016.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Katibu mkuuKiongozi Balozi Ombeni Sefue, maimu anatuhumiwa kwa kosa la matumizi mabaya ya fedha za umma.

Watumishi wengine wa mamlaka hiyo waliosimamishwa kazi kupisha uchunguzui ni pamoja na Mkurugenzi wa TEHAMA Joseph MAKANI, Afisa Ugavi Mkuu Bi Rahel MAPANDE, Mkurugenzi wa Sheria Bi Sabrina NYONI, na Afisa usafirishaji George NTALIMA.

Balozi Sefue amesema kuwa taarifa zilizomfikia Rais zinaonesha kuwa NIDA hadi sasa imetumia Shilingi bilioni 179.6 kiasi ambacho kinatajwa kuwa ni kikubwa.

Kufuatia ubadhirifu huo Rais ameelekeza Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) wafanye ukaguzi maalum wa manunuzi yote yaliyofanywa na NIDA.

Rais pia ameelekeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali afanye ukaguzi maalum wa hesabu za NIDA, ikiwemo ukaguzi wa “value for money” baada ya kuthibitisha idadi halisi ya vitambulisho vilivyotolewa hadi sasa.

Rais vile vile ameelekeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ifanye uchunguzi kujiridhisha kama kulikuwa na vitendo vya rushwa au la.

Taarifa hiyo inasema kuwa aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwenye Serikali ya Awamu ya Nne, Mhe. Mahadhi Juma MAALIM ameteuliwa kuwa Balozi wa kwanza wa Tanzania nchini Kuwait, kufuatia uamuzi wa Serikali kufungua Ofisi ya Ubalozi katika nchi hiyo rafiki.

Katika hatua nyingine, Balozi Sefue ameagiza kurejshwa nchini baadhi ya mabalozi wa Tanzania katika nchi mbalimbali.

Mabalozi hao ni pamoja na Bi Batilda Salha BURIANI, aliyeko Tokyo, Japan na Dkt. James Alex MSEKELA, aliyeko Rome, Italia huku akimrejesha Balozi wa Tanzania aliyeko London, Uingereza, Bwana Peter Allan KALLAGHE katika Wizara ya Mambo ya Nje, atakapopangiwa kazi nyingine.

Rais pia ametengua uteuzi wa Eng. Madeni Juma KIPANDE kabla hajathibitishwa kwenye cheo cha Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi kutokana na utendaji kazi usioridhisha.

Taarifa kamili iko hapa;- ...PDF