Jumamosi , 5th Oct , 2019

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemwagiza Kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Singida, Bw. Adili Elinipenda, amchunguze Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mkalama, Bw. Godfrey Sanga kwa matumizi mabaya ya fedha za umma.

Waziri Mkuu

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo jioni (Jumamosi, Oktoba 5, 2019), wakati akizungumza na madiwani na watumishi wa Halmashauri hiyo kwenye mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa Halmshauri hiyo.

Amezitaja baadhi ya tuhuma alizonazo ni kujilipa posho ya safari mwezi March mwaka huu bila kusafiri, kuwasainisha watumishi wa chini yake vocha na kisha kuwapa ‘asante kidogo’ kwa madai fedha hizo zinaenda mkoani, kujilipa stahiki kabla ya wakati na kuagiza gari liende gereji kwa matengenezo bila nyaraka zozote.

“Kuna watumishi wanne uliwaambia wasaini vocha ya sh. 1,320,000. Hii ni kwa safari iliyopangwa kati ya tarehe 15 na 24 Septemba, mwaka huu; ukawapa asante ya sh. 30,000 ukidai kuwa zinatakiwa mkoani. RAS ni kweli hela hiyo ililetwa mkoani?” Alihoji Waziri Mkuu na kujibiwa na Katibu Tawala wa Mkoa, Dkt. Anjelina Lutambi kwamba hakutoa hayo maagizo.

Alipoulizwa Mweka Hazina wa Wilaya hiyo, Bw. Peniel Mbula kwamba fedha alilipwa nani, mweka hazina huyo alijibu kwamba alikuwa Dodoma kikazi. Mhasibu aliyekaimu nafasi yake, Bi. Lulu Hamadi aliwataja watumishi hao kuwa ni Stella Mawa, Godfrey Mnubi, Richard Laizer na Method Kafuku.

 Waziri Mkuu aliwasimamisha watumishi hao na kuwauliza walilipwa hiyo posho ili waende wapi lakini walikosa majibu. Ndipo akawaeleza kwamba walimkabidhi Mkurugenzi na wakalipwa asante ya sh. 30,000.

 Alipoulizwa kuhusu malipo ya sh. 1,090,000 ambayo yalilipwa Septemba 9, mwaka huu yalikuwa ya nini, Mkurugenzi huyo alijibu kuwa ni ya stahiki zake za kila mwezi ambapo kati ya hizo, sh. 600,000/- ni za malipo ya nyumba; sh. 230,000  ni za umeme na sh. 260,000 ni za simu. Lakini hakuweza kujibu ni kwa nini amejilipa kabla mwezi haujaisha.

Kuhusu gari la elimu lenye namba za usajili STK 913 lililopelekwa gereji kupakwa rangi kwa gharama ya sh. milioni saba, Waziri Mkuu alitaka aoneshe dokezo lililotumika kupitisha idhini hiyo na malipo hayo lakini akajibiwa kwamba hakuna utaratibu wa kuandika dokezo pindi magari ya Halmashauri yanapoenda kufanyiwa matengenezo bali wanapeana taarifa kwa mdomo tu.

“Kamanda wa TAKUKURU leta maafisa kutoka mkoani waje wafanye ukaguzi wa kila jambo ambalo limeainishwa. Hatuwezi kuacha Halmashauri iendeshwe kienyeji bila kufuata taratibu. Mkalama inaonekana chafu kumbe tatizo ni mtu mmoja, mnasaini vocha halafu mnamsingizia RAS,” alimaliza.