Jumamosi , 8th Dec , 2018

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Albert Chalamila, ameagiza kuanza kwa msako na uhakiki wa vibali vya wamiliki wa silaha kwenye mkoa wake, lengo likiwa ni kudhibiti vitendo vya kiuhalifu vinavyotokana na matumizi mabaya ya silaha.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Albert Chalamila.

Mkuu wa Mkoa Chalamila ametoa agizo hilo kwa Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya mbele ya Kamanda wa Polisi Mkoa huo Matei, muda mfupi baada ya kukabidhi msaada binafsi wa magari mawili yenye thamani zaidi ya milioni 20 aliyotoa kwa jeshi hilo.

Chalamila amedai wapo wafanyabiashara wakubwa wanamiliki silaha kinyume cha taratibu na inawezekana matumizi yake yakawa mabaya pia, hivyo hiyo ikawa ni moja ya sababu inayochangia kuwa na ongezeko kubwa la vitendo vya uhalifu.

RPC inakupasa kutangaza upya zoezi la uhakiki wa silaha, anzia Chunya ambako kuna machimbo ya madini, kila mwenye silaha aeleze anaimiliki kwa ajili ya shughuli gani na tuone kama vibali vyake ni halali maana wakati mwingine watu wanajisahau sana,” amesema Chalamila.

Hivi karibuni Mkoa  huo uliingia kwenye sintofahamu baada ya wamachinga wa soko la Mwanjelwa wakitangaza mgomo kwa kile walichokidai kupinga amri ya Mkuu wa Mkoa kuhamishwa kwenye maeneo yao ya kazi.