Jumanne , 19th Jan , 2021

Serikali mkoani Geita imeuagiza uongozi wa shule ya sekondari ya Geita Islamic, ifikapo kesho asubuhi iwasilishe stakabadhi za malipo ya mitihani ya wanafunzi, baada ya Mwalimu Mkuu wa shule hiyo kukiri kula ada za mitihani ya Taifa ya wanafunzi wa kidato cha Pili na cha Nne.

Afisa Elimu wa mkoa wa Geita, Arnold Msuya

Akizungumza hii leo Januari 19, 2021, Afisa Elimu wa mkoa wa Geita, Arnold Msuya, amesema kuwa kitendo cha mwalimu huyo kula ada hizo, kimepelekea wanafunzi hao kukosa matokeo yao yaliyotangazwa hivi karibuni na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), ambapo kutokana na hali hiyo akaelekeza suala hilo lishughulikiwe na wanafunzi wapate matokeo yao.

"Tulipokea malalamiko kutoka kwa wazazi wa wanafunzi hao kwamba walilipa ada ya mitihani lakini matokeo ya watoto wao hayakutoka, nimemuelekeza mmiliki wa shule hiyo ifikapo kesho saa 4:00 asubuhi alete risiti za malipo ili matokeo yao yatoke, kama mkuu wa shule alipokea ada na akatoweka nazo hilo si jukumu la mzazi tena ni jukumu la mwenye shule aliyeruhusu fedha zikusanywe na kuwekwa mfukoni", amesema Arnold.

Kwa upande wake, Meneja wa shule hiyo Mussa Mnyita, amesema kuwa wazazi walikamilisha malipo hayo kutokana na changamoto ya mwalimu huyo kutolipa malipo hayo NECTA na kwamba uongozi wa shule utawajibika kulipa malipo hayo.