Ijumaa , 3rd Jan , 2020

Leo Januari 3, 2020, imefanyika ibada ya kuuga mwili wa mama yake mzazi na Mwandishi wa Habari, anayekabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi, Erick Kabendera, Verdiana Mujwahuzi, iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la Mt Francis Xaviel Chang'ombe, jijini Dar es Salam.

Pichani ni Erick Kabendera akifuta machozi, kulia na mama yake mzazi Verdiana Mujwahuzi enzi za uhai wake.

Akisoma ujumbe ulioandikwa na Erick Kabendera kwa watu wote walioshiriki katika ibada ya mazishi ya mama yake mzazi, Mbunge wa Kigoma Mjini, na Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, ameeleza namna ambavyo Erick anapitia kipindi kigumu cha kuondokewa lakini pia kunyimwa nafasi ya kumpa heshima za mwisho mama yake.

"Kuna mama mmoja, anafariki mara moja, msiba mara moja, uchungu wa kuondokewa na mama ni mkubwa sana, hasa anapokuwa ameondoka na umeshindwa kumuaga kama ilivyotokea kwangu, hata hivyo nimefarijika kwa Watanzania wote walioguswa na msiba huu bila kujali itikadi zao za kisiasa na kidini na kunisaidia kumsitiri Mama yangu" ameandika Kabendera.

Aidha Kabendera aliongeza kuwa, "Upendo huu umeonyesha nchi ambayo nimeipenda na naipenda kutoka moyoni, shukrani za dhati ziwafikie watu wote kwa upendo wao na ushiriki wao kufanikisha msiba wa Mama yangu, Mwenyezi Mungu na awabariki sana na kuwaongezea pale mlipopunguza kwa ajili yangu Mtuombee".

Mama wa Erick Kabendera alifariki dunia siku ya Disemba 31, 2019, katika hospitali ya Amana alikokuwa akipatiwa matibabu, na mwili wake umesafirishwa kupelekwa mkoani Kagera kwa ajili ya mazishi. Mungu ailaze Roho ya Marehemu Verdiana Mujwahuzi mahala pema Amina.