Jumatatu , 29th Mar , 2021

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo, ametangaza utaratibu kwa wahitimu wa kidato cha nne mwaka 2020 wanaotaka kubadilisha ‘Combination’ kidato cha tano na kozi za vyuo vya elimu ya ufundi kufanya hivyo kupitia mfumo wa kieletroniki.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo.

Akiongea leo Machi 29, 2021 kwenye ofisi za Wizara hiyo jijini Dodoma, Jafo amesema wameanzisha tahsusi mpya zikiwemo zitakazo fundisha Kiswahili, Kifaransa na Kichina ili kuongeza upana wa fani ikiwemo wakalimani kuwa wengi. Amesema tahsusi hizo zimewekwa maalumu kwenye shule mbili za wasichana na wavulana.

''Mfumo huu mpya wa kielektroniki unawawezesha wanafunzi kubadili tahsusi ambazo wamechagua awali pengine kwa kutokuwa na uhakika au kwa kushauriana na wazazi au walezi ama pia kwa sababu nyingine yoyote'', amesema Jafo.

Aidha amefafanua kuwa zoezi hilo litafanyika kuanzia Machi 29, 2021 hadi Aprili 11, 2021 saa 6:00 usiku.

''Wanafunzi wanaotaka kufanya mabadiliko wanatakiwa kuingia kwenye mfumo wa uchaguzi wa wanafunzi unaopatikana katika anuani ya selform.tamisemi.go.tz.'', ameongeza Waziri Jafo.

Tazama Video hapo chini