Jumapili , 28th Sep , 2025

Upigaji kura wa mapema ulianza Alhamisi, lakini watu wengi walipiga kura jana Jumamosi.

Nchi ya Ushelisheli inatarajia kurudia uchaguzi mkuu baada ya kukosekana kwa mshindi wa moja kwa moja katika uchaguzi wa urais,hivyo nchi hiyo itapiga kura ya marudio kati ya wagombeaji wakuu wawili, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na halmashauri ya kusimamia uchaguzi.

Katika matokeo ya uchaguzi uliofanyika, Mpinzani Patrick Herminie amepata 48.8% ya kura, wakati mgombea, Wavel Ramkalawan, akipata 46.4%, kulingana na matokeo rasmi. Mgombea anahitaji kushinda zaidi ya 50% ya kura ili kutangazwa mshindi.Tarehe ya marudio ya uchaguzi bado haijatangazwa.

Herminie anawakilisha chama cha United Seychelles, ambacho kilitawala siasa kwa miongo kadhaa nchini humo kabla ya kupoteza mamlaka miaka mitano iliyopita. United Seychelles kilikuwa chama tawala kutoka 1977 hadi 2020.

Kwa upande wake rais Wavel Ramkalawan kutoka chama cha Linyon Demokratik Seselwa anatafuta muhula wa pili kama kiongozi wa nchi hiyo ndogo zaidi barani afrika, akijaribu kuzuia United Seychelles kurejea madarakani. chama chake tawala cha linyon demokratik seselwa kilifanya kampeni ya kufufua uchumi, maendeleo ya kijamii na uendelevu wa mazingira.

Visiwa hivyo vyenye visiwa 115 katika Bahari ya Hindi vimekuwa ni sehemu inayovutia kwa watalii kwenda kupumuzika, hivyo kuifanya Shelisheli kuwa kileleni mwa orodha ya nchi tajiri zaidi za Afrika kwa pato la taifa kwa kila mtu, kulingana na Benki ya Dunia.