"Mtanisamehe lugha yangu" - Magufuli

Alhamisi , 22nd Feb , 2018

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli amefunguka na kusema kuwa yeye si mwanasiasa mzuri ndiyo maana lugha yake siku zote si nzuri.

Magufuli amesema hayo leo Februari 22, 2018 wakati akihotubia katika mkutano wa 19 wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao unaendelea sasa Kampala nchini Uganda ambapo Marais wa nchi hizo wamekutana huko kujadili mambo mbalimbali ambapo Rais Magufuli amewataka viongozi hao kuangalia changamoto mbalimbali ambazo zinazikabili nchi hizo.

"Mtanisamehe lugha yangu siyo nzuri kwa kuwa mimi siyo mwanasiasa mzuri, tunataka kutengeneza viwanda yaani kuzifanya nchi zetu ziwe za viwanda tutaweza kushindana na nchi ambazo gharama yake ni 0.12 wakati sisi ni zaidi ya mara kumi ya hiyo hayo ni maswali ambayo sisi ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kila mmoja wetu lazima tujiulize je tutafika hapo hizo ndiyo changamoto lakini pia gharama za umeme zinasababisha gharama za uzalishaji kuongezeka na kupelekea pato la taifa kushuka kwa asilimi 2 na kuongeza gharama za uzalishaji kwa asilimia 40 sasa kama pato la taifa linashuka kwa asilimia 2 na gharama ya usafirishaji zinakuwa kwa asilimia 40 hizo nazo ni changamoto. Tunapopeleka miradi kama hii ni lazima ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki viongozi, mawaziri, makatibu wakuu na sisi Marais ni lazima haya tuyaweke manani je tutaweza kushindana ikiwa gharama za uzalishaji katika nchi za Afrika Mashariki ni asilimia 40 kubwa ukilinganisha na mahali pengine" 

Rais Magufuli aliendelea kutoa maelezo katika mkutano huo 

"Tujiulize kwenye mwaka 2014 tulifanikiwa zaidi kwenye kuunganisha barabara tujiulize kwanini miradi mingine haikufanikiwa, tulitakiwa kuangalia faida na hasara kwamba kwanini sisi marais wa Afrika Mashariki tunapitisha miradi ila utekelezaji wake haupo, kwa sababu kama kuna miradi 14 tu iliyokamilika mingine ipo kwenye mchakato karibia saba kulingana na ripoti wakati tulipeleka mingi ina maana kuna tatizo, sasa viongozi tulitakiwa kuangalia hayo matatizo badala ya kuja tena hapa na kuomba tena kitu wakati tunajua katika miradi hii tuliyoomba kwa vyovyote haiwezi kutekelezwa yote" alisema Magufuli 

Kuhusu masuala ya Afya pia Rais Magufuli aligusia na kusema kuwa Tanzania kwa miaka miwili wamejaribu kuongeza bajeti ya afya kutoka bilioni 31 mpaka bilioni 200 na kitu aidha Rais Magufuli amesema kuwa kama nchi hizo zitatumia vizuri mapato ya ndani na kujibana itasaidia nchi hizo kuweza kuendesha baadhi ya vitu na maendeleo kupitia fedha zao za ndani.

"Mimi nitoe wito wote ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki tubadilishe mawazo yetu zile fedha tunazozikusanya, yale mapato tunayoyapata tuyatumie vizuri ili baadhi ya miradi tuifanye vizuri sisi wenyewe, tunahitaji development partners na wanafanya kazi vizuri sana, tunahitaji PPP lakini tunatakiwa na sisi ndani ya Afrika Mashariki zile resources tunazopata tuzitumie vizuri na sema hili kwa uzoefu mdogo niliokuwa nao kwa miaka miwili, tuliomba sana fedha kwa ajili ya kujenga reli ya standard gauge hatukupata na muda mwingine masharti yalikuwa juu tukaamua ngoja tuanze sisi wenyewe, tumekusanya hela kutoka hizo hizo za Watanzania sasa hivi tunajenga reli kilomita 726 na fedha zipo hata leo zipo hata kandarasi angeomba leo tungemlipa zote hilo limewezekana kwa sababu tumebana" alisema Rais Magufuli