Jumapili , 2nd Dec , 2018

Rais John Magufuli leo Desemba 2, 2018 amezindua na kuweka jiwe la msingi ujenzi wa visima vikubwa vya maji zaidi ya 20 jijini Arusha.

Rais Dkt. John Magufuli.

Rais amesema kuwa mradi huo utakaogharimu shilingi bilioni 520, unahusisha visima vya kuchimbwa na kumaliza tatizo la maji katika Jiji hilo, na zimekopwa katika Benki ya Maendeleo ya Afrika, hivyo zitalipwa na Watanzania wote kupitia kodi.

"Serikali imekopa bilioni 520 kutoka Benki ya maendeleo ya Afrika, kwa ajili ya Arusha ili kutekeleza mradi wa maji, hizi hela zitalipwa na Watanzania wote, na tumezileta kwa wale wale wanaoitukana serikali, na yote ni kwasababu maendeleo hayana chama", amesema Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Isack Kamwele kutosita kuwafukuza wakandarasi wakishindwa kutekeleza mradi huo kwa wakati, "Waziri usiogope kufukuza wakandarasi, kumbuka hata mimi nimewahi kuwa Waziri wa Ujenzi na sikusita kutimua wakandarasi wasiotekeleza miradi, wakaanza kuniombea laana, na hazikunipata kwakuwa Mungu anapenda maendeleo ya haki, wewe fukuza tu".

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amesema mradi huo ukikamilika uhaba wa maji Jiji la Arusha utapungua kwa kiasi kikubwa.