Alhamisi , 18th Jun , 2020

Mtia nia wa kugombea nafasi ya Urais kupitia CHADEMA, Leonard Manyama, amesema kuwa miongoni mwa majina 11 ya watia nia yaliyotangazwa na chama hicho, haoni hata mmoja ambaye anaweza akamzidi na hivyo yeye ndiyo atapewa ridhaa ya kupepeperusha bendera ya chama.

Leonard Manyama, Mtia nia wa kugombea nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CHADEMA.

Manyama ameyabainisha hayo leo Juni 18, 2020, wakati wa mazungumzo maalumu na EATV&EA Radio Digital, ambapo pia amevitaja vipaumbele vyake katika siku 100 za kwanza pale atakapokuwa amechaguliwa na wananchi, ikiwemo kujenga Taifa lenye umoja na mshikamano, kwa madai ya kuwa vitu hivyo havijafanyika tangu mfumo wa vyama vingi uanze hapa nchini.

Aidha amesisitiza kuwa ataliunganisha taifa katika masuala ya Mungu, uhuru wa vyombo vya habari na kwamba katika utawala wake hatoogopa kunyoshewa vidole kwa kuweka usawa kwa kila mtu

"Wagombea wote waliojitokeza kutangaza nia wana uwezo na sifa stahiki, mimi ninategemea kwa kila mmoja wetu anaweza kuchaguliwa na chama, na katika wote tuliochaguliwa sina ninayemhofia ila ninawaheshimu wanachama wenzangu" amesema Manyama.

CHADEMA tayari imekwishawatangaza watia nia 11 wa kugombea nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiwemo Lazaro Nyalandu, Tundu Lissu, Freeman Mbowe, Peter Msigwa, Richard Simba, Shaban Msafiri na wengine.