Jumatano , 21st Aug , 2019

Kufuatia kuwepo kwa maswali kadhaa ya watu kuhoji,  sababu inayopelekea majeruhi wa ajali ya moto waliohamishiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kufariki kila iitwapo leo, uongozi wa hospitali hiyo umebainisha chanzo cha vifo hivyo.

Hospitali ya Taifa ya Muhimbili

Daktari bingwa wa upasuaji katika Hospitali hiyo  Dk. Laurian Rwanyuma, amesema kuna weza kukawa kunautofauti wa vifaa vinavyopatikana katika hospitali zilizo nje ya nchi, lakini tatizo kubwa lililojitokeza ni wagonjwa kuungua sehemu kubwa ya miili yao.

''Katika suala hili wataalamu wapo, vifaa vipo tunaweza kuzidiana na nchi zingine za Ulaya, lakini tatizo kubwa lililojitokeza ni wagonjwa kuungua sehemu kubwa za miili, wameungua asilimia 80, 90 hadi 100, lakini tunapigana na maisha ya binadamu, hatuwezi kuhukumu kwamba huyu hawezi kutibiwa kwa sababu hiyo iko nje ya maadili ya kidaktari'' amesema Dk Rwanyuma.

Ufafanuzi huo umetolewa leo Agosti 21, ambapo hadi leo idadi ya vifo vilivyotokana na ajali hiyo vimefikia 100, ambapo hospitali hiyo imesalia na wagonjwa 15 kati ya wale majeruhi 47 iliyokuwa imewapokea kutoka mkoani Morogoro.