Jumapili , 19th Jan , 2020

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, George Simbachawene, amesema kuwa Mwaka Mpya wa Panya ulioadhimishwa usiku wa kuamkia leo Januari 19, 2020, utakuwa na mafanikio kwa Taifa, hii ni kutokana na uwepo wa mahusiano mazuri kati ya Tanzania na China.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, George Simbachawene.

Waziri Simbachawene ameyabainisha hayo wakati wa hafla ya kuadhimisha Mwaka Mpya wa Kichina uliopewa jina la mwaka wa Panya, ambapo kwa mwaka jana waliuita mwaka wa Nguruwe.

"Mwaka huu wa Panya kwa mila za Kichina ni mwaka ambao mnausherehekea huku mkitafakari mliyoyafanya mwaka uliopita, na mimi naamini kwa kuwa Panya ni mnyama mjanja sana, naamini Mwaka huu utakuwa wa mafanikio makubwa kati ya Tanzania na China" amesema Waziri Simbachawene.

Kwa upande wake Balozi wa China Nchini Tanzania, Wang Ke, amesema kuwa Serikali ya nchi hiyo itaendelea kushirikiana na Tanzania katika ukuzaji wa maendeleo na kwamba katika kipindi cha Mwaka huu mpya, wataendeleza mikakati ya kupunguza umasikini pamoja na kujenga jamii yenye uchumi imara.