Jumatano , 4th Dec , 2019

Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe, imempandisha kizimbani Emanuel Mbembela (42) mwalimu wa Shule ya Sekondari Nambizo, kwa kumbaka na kumpa ujauzito mwanafunzi  wa kidato cha nne.

Akimsomea mashtaka hayo mwendesha mashtaka wa Serikali, Gibson Tawale, mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo Tumain Maleko, amesema mshtakiwa ametenda kosa hilo Julai 30, 2019, katika Kijiji Cha Isenzanya Kata ya Nambizo, wilayani Mbozi.

Mwendesha mashitaka wa Serikali Gibson Tawale ameongeza kuwa mshtakiwa anakabiliwa na mashtaka matatu, huku la kwanza ni kumbaka mwanafunzi, kosa la pili kumpa ujauzito na kosa la tatu kumkatisha masomo mwanafunzi.

Mwendesha mashtaka wa Serikali Gibson Tawale, amesema kuwa upelelezi unaendelea juu ya tukio hilo na ameomba tarehe nyingine kwa ajili ya kusoma hoja za awali .

Kwa upande wake Mwalimu Emanuel Mbembela, amekana shitaka hilo na Hakimu wa mahakama hiyo Tumain Maleko ameahirisha shauri hilo mpaka Desemba 17, 2019.