
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dkt Adelardus Kilangi.
Dkt Kilangi ameyabainiha hayo leo Februari 4, 2020, Bungeni Dodoma, katika Mkutano wa 18 wa Bunge la 11, Kikao cha Sita, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Zainabu Katimba, alipouliza swali kuhusu matukio ya ubakaji kwa watoto.
"Pendekezo la kuhasiwa kwa mbakaji tutavunja katiba kwa sababu, katiba inaeleza ni marufuku mtu kuteswa kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazomtweza/kumdhalilisha, nafikiri adhabu zilizopo zinajitosheleza kwa sasa" amesema Dkt Kilangi.
Kwa upande wake Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, akiongezea katika jibu la Mwanasheria Mkuu, ameendelea kuwasisitiza wazazi na walezi, kujenga ukaribu na watoto wao ili kuweza kuwaambia pale wanapokutana na vitendo vya ukatili.
"Hata tuwe na sheria kali kiasi gani hatutamaliza tatizo la ubakaji na ulawiti kwa watoto na wanawake, nitoe msisitizo kwa wazazi na jamii kutimiza wajibu wetu wa malezi na ulinzi kwa watoto, mtoto anabakwa miezi mitatu bila mzazi kujua unajiuliza je huyu ana wazazi?" amesema Waziri Ummy.