Jumatatu , 22nd Apr , 2019

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Agrey Mwanri amefafanua kauli yake ya kumtaka Mungu amshukuru Rais Magufuli ambayo aliitoa hivi karibuni ambapo amesema kauli hiyo ililenga kumshukuru kiongozi huyo kwa mambo anayoyafanya kwa sasa katika kuleta maendeleo.

Akizungumza na waandishi habari Mjini Tabora Mwanri amedai suala hilo, lilipata tafsiri potofu kwa baadhi ya watu hasa kupitia mitandao ya kijamii.

"Nilichokuwa nalenga pale ni hiki hapa mfano nitoe kwenu kwa waandishi wa habari mara nyingi mnatuunga mkono Serikali katika kuleta maendeleo ya Tabora, inafika mahali katika kuzungumza na waandishi wa habari nawaambia uwezo wa kushukuru sina, nitachofanya kumuomba mwenyezi Mungu awashukuru kwa kazi nzuri mnayofanya." amesema Mwanri

Mwanri ameongeza kuwa "mimi nimekuwa nikiwaambia hata wananchi kuwa mimi siwezi kuwashukuru bali nitamwachia Mungu awashukuru, ila nilichosema siku ile ni nilimaanisha Rais Magufuli anafanya kazi nzuri na ni mambo makubwa yaliyotufurahisha mioyo yetu, ninachoweza kusema na kufanya ni kumuomba Mungu atusaidie kumshukuru Rais Magufuli, japo jambo lile lilipata tafsiri potofu"

"Ila nilichojifunza inapopelekwa habari kama ile masikio yanayopokea ni mengi usifikiri hata kama uko sawa ukafikiri utapokea kwa hisia hivyohivyo, kama masikio mengi yalipokea jambo hilo kwa tofauti sina cha zaidi ya kuomba msamaha kwa sababu nimeshafafanua na mimi ambao walininukuu vibaya natangaza nimeshawasamehe, ni Mungu peke yake hakuna binadamu atakayeweza kuchukua nafasi ya Mungu, nitakuwa nimechuja sana nikiamini binadamu anaweza kuchukua nafasi ya Mungu" amesema Mwanri

Mwanzoni mwa mwezi Aprili Mkuu wa huyo wa Mkoa alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari nchini juu ya kutoa kauli ambayo alieleza kuwa anamuomba Mungu amshukuru Rais Magufuli hali iliyomfanya kuzua taharuki kwenye mitandao ya kijamii.