Jumatano , 15th Mei , 2019

Aliyekuwa Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba amedai ushindi ambao wamekuwa wakiupata Chama Cha Mapinduzi hautokani na kupendelewa na Wakurugenzi wa ambao ni wasimamizi wa uchaguzi.

Aliyekuwa Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba.

Mwigulu ametoa mkauli hiyo ikiwa ni siku chache baada ya Mahakama kuu ya Tanzania kubatilisha sheria inayowapa Mamlaka Wakurugenzi kusimamia Uchaguzi huku baaadhi yao wakiwa wafuasi wa vyama vya siasa, kesi ambayo ilifunguliwa na Mwanaharakati Bob Chacha Wangwe.

Akijibu tamko la ACT - Wazalendo ambao walihoji juu ya CCM kupata ushindi wa upendeleo, Mwigulu Nchemba amesema, "ushindi wa CCM hautokani na na hisani ya Wakurugenzi bali ni kura za wananchi. CCM ina heshima ya urithi wa ukombozi wa nchi hii ambayo chama kingine chochote hakina".

"CCM ina mtandao wa wanachama na muundo wa kitaasisi kuliko chama chochote kile nchini, CCM mara zote imekuwa na ilani bora, sera bora, na wagombea bora kuliko wengine." amesema Mwigulu Nchemba.

"Acheni Wanasheria wafanye ya kisheria, wanasiasa msitafute huruma na visingizio, wakati wengine hamna hata wanachama wanaofikia idadi ya wanachama wa CCM wa kijiji kimoja, hata mkisimamia wenyewe uchaguzi CCM ina wapiga kura itashinda", amemalizia katika maoni yake Mwigulu Nchemba.