Ijumaa , 12th Feb , 2016

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mhe. Mwigulu Nchemba amemsimamisha kazi mkuu wa mnada wa Pugu na watumishi wengine kwa ubadhirifu na ukwepaji kodi ikiwa ni pamoja kuwaingiza ng'ombe kwenye machinjio bila kibali halali.

Waziri wa Kilimo,Mifugo na Uvuvi Mwigulu Nchemba,akiongoza na Mbunge wa Jimbo la Ukonga Mwita Waitara katika Machinjio ya Ukonga Mazizi Jana usiku.

Waziri Mwigulu amechukua hatu hiyo baada ya kufanya ziara katika machinjio ya Ukonga Mazizi jana usiku na kukamata ng'ombe 200 wakiwa wanaingizwa kwenye machijio bila kibali halali na ni ng'ombe 20 pekee ndiyo wana kibali cha kuchinjwa.

Waziri huyo amesema kuwa kati ya ng'ombe 200, ng'ombe 180 hawajalipiwa ushuru hivyo ameviagiza vyombo vya dola usiku huo huo kuwakamata watumishi wote waliokuwa zamu na kuwafikisha mahakamani haraka iwezekanavyo na hatua nyingine za kiofisi zitafuata.

Mhe. Mwigulu amesema kuwa serikali inakosa kuingiza mapato yake kutokana na watu wachache kuhujumu kodi ya serikali ikiwa ni pamoja na kuchukua ushuru bila kupeleka mahali husika na kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.

Katika ziara hiyo waziri huyo aliongoza na mkurugenzi wa manispaa ya Ilala, na mbunge wa jimbo la Ukonga Mhe. Waitara Mwita ambapo aliwashukuru kwa kutoa ushirikiano kwa kufanikisha kubaini uhalifu huo unaofanywa usiku wa manane na kuisababishia serikali hasara.