Jumatatu , 1st Mar , 2021

Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema miongoni mwa mambo aliyoyabaini ndani ya muda mfupi tangu ateuliwe kuwa Rais wa Zanzibar ni wanachi kukosa sehemu ya kuwasilisha changamoto zao.

Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Akizungumza katika Kongamano la kujadili Matumizi ya Sekta ya Mawasiliano ya Habari katika kuijenga Zanzibar mpya, mjini Unguja ameeleza kwa muda mrefu wameimarisha mifumo ya taarifa kupelekea kwa wananchi lakini bado hakuna mifumo madhubuti ya kupokea taarifa kutoka kwao.

“Mimi binafsi miongoni mwa mambo niliyoyabaini katika kipindi hiki kifupi tokea kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar ni changamoto nyingi zinazowakabili wananchi na kwa bahati mbaya wanakosa sehemu ya kuziwasilisha changamoto hizo na kupata ufumbuzi wa haraka” amesema Rais Mwinyi

Aidha Rais Mwinyi ametoa maagizo kwa wakuu wa  Taasisi kukutana na wanahabari na kujadili namna ya kufanikisha utoaji wa habari huku akiwahimiza wanahabari kushirikiana na serikali kupiga vita ufisadi, udhalilishaji, rushwa na vitendo vyote vya uvunjifu wa sheria.

“Nachukua nafasi hii kuwaagiza wakuu wa Taasisi kukutana na maafisa habari na maafisa uhusiano waliopo kwenye taasisi zao na kuweka mikakati yao kwa pamoja namna ya kuwasilisha utoaji wa habari katika taasisi zao sambamba na kutatua changamoto zao.”