Alhamisi , 26th Mei , 2022

Mahakama ya wilaya ya Lindi, imemhukumu mkazi wa Kijiji cha Namkongo,Kata na Tarafa ya Mipingo, mkoani humo Salum Mtopa mwenye umri wa miaka 70 kifungo cha miaka 90 gerezani, baada ya kukutwa na hatia kwa makosa matatu, likiwemo kumiliki shamba linalohusika na kilimo cha bangi.

Nyundo ya Hakimu

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo,Maria Batraine, baada ya kuridhishwa pasipo shaka na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo,Hakimu Batraine alimuuliza mshtakiwa kama ana sababu za msingi itakayoishawishi Mahakama isimpe adhabu kali, aliomba isimpe adhabu kali kwa madai ni mkosaji wa mara ya kwanza,umri wake umeshakwenda,pia anayo familia  inayomtegemea mke na wajukuu watano.

"Mhe, Hakimu kama unavyoniona mimi sasa ni mzee na nina wajukuu wananitegemea,ukinipa adhabu kubwa watakosa huduma zangu," Aliomba Mtopa.

Baada ya utetezi huo,Hakimu alimuuliza mwendesha mashtaka, Mkaguzi John Ijumba, kama anazo kumbukumbu ya makosa ya zamani kwa mshitakiwa na kujibu hana, huku akiiomba Mahakama impe mshtakwa adhabu kali ili iwe fundisho kwake na wengine walio na tabia ya aina hiyo.

Hakimu Batraine akitoa hukumu katika kesi hiyo ya Jinai Namba 46/2021,kupitia vifungu 11 (i)(b) na 11 (1) (a) kama vilivyofanyiwa marejeo 2019,alisema makosa aliyofanya mshitakiwa yapo kwa mujibu wa sheria, hivyo hana uwezo wa kubadilisha,na kumhukumu kosa la kwanza kukutwa na nangi kutumikia kifungo cha miaka 30 Jela.

Kosa la pili kushiriki kukutwa na mbegu kutumikia kifungo cha miaka (30),pa adhabu ya aina hiyo alipewa kwa kosa la tatu la kusafirisha bangi kutumikia gerezani kifungo cha miaka (30) na kufanya Jumla ya miaka kuwa 90 na kwa vile adhabu zinakwenda kwa pamoja mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka (30).

Aidha,mshitakiwa ameambiwa nafasi ya kukata rufaa ipo wazi kama atakuwa hakuridhishwa na hukumu iliyotolewa na Mahakama hiyo ya wilaya.

Mshtakiwa alifanya kosa hilo Julia 20, 2021, huko Namkongo baada ya kukutwa akiwa na jumla ya kilogram 151.99 za madawa ya kulevya aina ya bangi, kati ya hizo, kilogramu 132.94 ni mbegu, pia alikutwa akimiliki shamba la bangi lenye ukubwa wa ekari 5.54.