Ijumaa , 5th Sep , 2014

Tabia ya baadhi ya vijana kupenda kwenda kwenye ngoma za usiku na zisizo na maadili maarufu kama kigodoro na kangamoko, imetajwa kuchangia ongezeko la maambuki ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Ukimwi miongoni mwa vijana wengi nchini Tanzania.

Afisa Uragibishi kutoka baraza la taifa la watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi NACOPHA Bi. Lilliane Chovenye, amesema hayo leo Jijini Dar es Salaam wakati wa mafunzo yaliyofadhiliwa na shirika la kimataifa la idadi ya watu UNFPA, mafunzo yanayotolewa kwa vijana waathirika wa UKIMWI, kuhusu afya ya uzazi, na namna vijana hao wanavyoweza kuwa wawazi kuhusu afya zao, pale wanapokwenda kupata tiba katika vituo vya kutolea tiba.

Kwa mujibu wa Bi. Chovenye, makundi ya vijana wanaokwenda kwenye ngoma hizo wamekuwa hawachukui tahadhari ya kufanya ngono salama kama vile kutumia kondomu, licha ya kwamba wengi wao wanakuwa wametumia vileo ambavyo huwafanya wasiwe makini wakati wa mapenzi.

Kwa upande wake, mmoja wa waathirika hao msichana Rosemary Sabinus amesema vijana wengi nchini wamejikuta wakipata maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutokana na kutozingatia mafunzo wanayopata kutoka kwa wazazi, walezi pamoja na watu waliowazidi umri, hasa mafundisho yanayowataka kutojihusisha na ngono zembe.

Bi. Sabinus amewataka vijana wenzake kuacha ukaidi wanapopewa maelekezo kutoka kwa wazazi au watu waliowazidi umri, hasa kwa masuala ya msingi kwao ikiwemo kuchukua tahadhari dhidi ya Ukimwi.

Mafunzo hayo yanayofadhiliwa na UNFPA, yanalenga kupunguza maambukizi kwa makundi ya vijana kuanzia miaka kumi na nne hadi ishirini na nne, kundi ambalo linaonekana kuwa katika hatari zaidi ya kupata na kusambaza maambukizi mapya ya virusi vya ukwimi.